11. Msimwogope mfalme wa Babeli, mnayemwogopa; msimwogope, asema BWANA; maana mimi ni pamoja nanyi, niwaokoe, na kuwaponya na mkono wake.
12. Nami nitawapa rehema, kwamba awarehemu ninyi, na kuwarudisha mkae katika nchi yenu wenyewe.
13. Lakini mkisema, Hatutaki kukaa katika nchi hii; msiitii sauti ya BWANA, Mungu wenu;
14. mkisema, La! Lakini tutakwenda nchi ya Misri, ambayo hatutaona vita, wala kuisikia sauti ya tarumbeta, wala kuona njaa kwa kukosa chakula; nasi tutakaa huko;
15. basi, lisikieni neno la BWANA, enyi mabaki ya Yuda; BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ikiwa mwakaza nyuso zenu kuingia Misri, na kwenda kukaa huko;
16. basi, itakuwa, upanga mnaouogopa utawapata huko, katika nchi ya Misri, nayo njaa mnayoiogopa itawafuatia mbio huko Misri, nanyi mtakufa huko.
17. Haya ndiyo yatakayowapata watu wote waelekezao nyuso zao kwenda Misri, na kukaa huko; watakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesalia, au kuokoka katika mabaya nitakayoyaleta juu yao.
18. Maana BWANA wa majeshi Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama hasira yangu, na ghadhabu yangu, ilivyomwagwa juu ya hao wakaao Yerusalemu, ndivyo ghadhabu yangu itakavyomwagwa juu yenu, mtakapoingia Misri; nanyi mtakuwa apizo, na ajabu, na laana, na aibu; wala hamtapaona mahali hapa tena.
19. BWANA asema katika habari zenu, enyi mabaki ya Yuda, Msiingie Misri; jueni sana ya kuwa nimewashuhudia hivi leo.
20. Maana mmetenda kwa hila juu ya nafsi zenu wenyewe; kwa kuwa mmenituma kwa BWANA, Mungu wenu, mkisema, Utuombee kwa BWANA, Mungu wetu, ukatufunulie sawasawa na yote atakayoyanena BWANA, Mungu wetu, nasi tutayatenda;
21. nami nimewafunulia haya leo; lakini ninyi hamkuitii sauti ya BWANA, Mungu wenu, katika neno lo lote ambalo amenituma kwenu.
22. Basi, sasa jueni sana ya kuwa mtakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, katika mahali pale mnapopatamani kwenda na kukaa.