Yer. 4:2-13 Swahili Union Version (SUV)

2. nawe utaapa hivi, Kama BWANA aishivyo, katika kweli, na katika hukumu, na katika haki ndipo mataifa watajibariki katika yeye, nao watajitukuza katika yeye.

3. Maana BWANA awaambia hivi watu wa Yuda na Yerusalemu Ulimeni udongo katika konde zenu, wala msipande mbegu kati ya miiba.

4. Jitahirini kwa BWANA, mkaziondoe govi za mioyo yenu, enyi watu wa Yuda na wenyeji wa Yerusalemu; ghadhabu yangu isije ikatoka kama moto, ikawaka hata mtu asiweze kuizima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu.

5. Tangazeni katika Yuda, hubirini katika Yerusalemu, na kusema, Pigeni baragumu katika nchi, pigeni kelele sana, na kusema, Jikusanyeni pamoja, tukaingie katika miji yenye boma.

6. Twekeni bendera kuelekea Sayuni; kimbieni mpate kuwa salama, msikawie; kwa maana nitaleta mabaya toka kaskazini, na maangamivu makuu.

7. Simba ametoka katika kichaka chake, ndiye aangamizaye mataifa; ameanza kushika njia, ametoka katika mahali pake; ili aifanye nchi yako kuwa ukiwa, miji yako ifanywe maganjo, asibaki mwenyeji ndani yake.

8. Kwa sababu hiyo jifungeni nguo za magunia; ombolezeni na kulia kwa uchungu; kwa maana hasira kali ya BWANA haikugeuka na kutuacha.

9. Na katika siku hiyo itakuwa, asema BWANA, moyo wa mfalme utapotea, na moyo wa wakuu wake; na makuhani watastaajabu, na manabii watashangaa.

10. Nami nikasema, Aa, Bwana MUNGU! Hakika umewadanganya sana watu hawa na Yerusalemu, ukisema, Mtakuwa na amani lakini upanga umeingia katika nafsi za watu.

11. Wakati ule watu hawa na Yerusalemu wataambiwa neno hili, Upepo wa moto utokao katika vilele vya nyikani visivyo na miti, ukimwelekea binti ya watu wangu, hauwi upepo wa kupepeta, wala upepo wa kutakasa;

12. ni upepo wa nguvu kuliko hizo utakaokuja kwa ajili yangu; sasa mimi nitatoa hukumu juu yao.

13. Tazama atapanda juu kama mawingu, na magari yake ya vita yatakuwa kama kisulisuli; farasi zake ni wepesi kuliko tai. Ole wetu, kwa sababu tumeharibika.

Yer. 4