19. Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, Nawaogopa Wayahudi waliowakimbilia Wakaldayo, wasije wakanitia katika mikono yao, nao wakanidhihaki.
20. Lakini Yeremia akasema, La! Hawatakutoa. Nakusihi, uitii sauti ya BWANA katika hayo ninayokuambia; ndivyo itakavyokufaa, na nafsi yako utaishi.
21. Lakini kama ukikataa kutoka, hili ndilo neno ambalo BWANA amenionyesha;
22. Tazama, wanawake wote, walioachwa ndani ya nyumba ya mfalme wa Yuda, watatolewa na kuchukuliwa kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, na wanawake hao watasema, Rafiki zako walio karibu wamekudanganya, nao wamekushinda; na kwa kuwa miguu yako imezama matopeni sasa, wamegeuka na kurudi nyuma.
23. Na watawatoa wake zako, na watoto wako wote, na kuwachukua kwa Wakaldayo; wala wewe hutapona na mikono yao, bali utakamatwa kwa mkono wa mfalme wa Babeli, nawe utakuwa sababu ya kuteketezwa mji huu.
24. Ndipo Sedekia akamwambia Yeremia, Mtu ye yote asipate habari ya maneno haya, nawe hutakufa.
25. Lakini kama wakuu wakisikia ya kuwa nimenena nawe, nao wakija kwako, na kukuambia, Tufunulie sasa uliyomwambia mfalme; usimfiche, nasi hatutakuua; na pia uliyoambiwa na mfalme;
26. basi, utawaambia, Nalimwomba mfalme asinirudishe nyumbani kwa Yonathani, nisije nikafa humo.
27. Ndipo wakuu wakamwendea Yeremia, wakamwuliza; naye akawaambia sawasawa na maneno aliyoamriwa na mfalme. Basi wakaacha kunena naye; maana neno lile halikujulikana.