13. Basi wakamwinua Yeremia kwa kamba hizo, wakamtoa shimoni; naye Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi.
14. Kisha mfalme Sedekia akatuma watu, akamleta nabii Yeremia kwake, ndani ya maingilio ya tatu ya nyumba ya BWANA; mfalme akamwambia Yeremia, Nataka kukuuliza neno, nawe usinifiche neno lo lote.
15. Basi Yeremia akamwambia Sedekia, Kama nikikufunulia neno hilo, je! Hutaniua wewe? Tena, mimi nikikupa shauri wewe hutanisikiliza.
16. Basi Sedekia mfalme akamwapia Yeremia kwa siri, akisema, Kama BWANA aishivyo, yeye aliyetufanyia roho zetu, sitakuua, wala sitakutia katika mikono ya watu hao wanaokutafuta wakuue.
17. Ndipo Yeremia akamwambia Sedekia, BWANA, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama ukitoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, basi nafsi yako utaishi, wala mji huu hautateketezwa; nawe utaishi na nyumba yako;
18. bali ukikataa kutoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, basi, mji huu utatiwa katika mikono ya Wakaldayo nao watauteketeza, hata na wewe hutajiepusha na mikono yao.
19. Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, Nawaogopa Wayahudi waliowakimbilia Wakaldayo, wasije wakanitia katika mikono yao, nao wakanidhihaki.
20. Lakini Yeremia akasema, La! Hawatakutoa. Nakusihi, uitii sauti ya BWANA katika hayo ninayokuambia; ndivyo itakavyokufaa, na nafsi yako utaishi.
21. Lakini kama ukikataa kutoka, hili ndilo neno ambalo BWANA amenionyesha;
22. Tazama, wanawake wote, walioachwa ndani ya nyumba ya mfalme wa Yuda, watatolewa na kuchukuliwa kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, na wanawake hao watasema, Rafiki zako walio karibu wamekudanganya, nao wamekushinda; na kwa kuwa miguu yako imezama matopeni sasa, wamegeuka na kurudi nyuma.
23. Na watawatoa wake zako, na watoto wako wote, na kuwachukua kwa Wakaldayo; wala wewe hutapona na mikono yao, bali utakamatwa kwa mkono wa mfalme wa Babeli, nawe utakuwa sababu ya kuteketezwa mji huu.
24. Ndipo Sedekia akamwambia Yeremia, Mtu ye yote asipate habari ya maneno haya, nawe hutakufa.
25. Lakini kama wakuu wakisikia ya kuwa nimenena nawe, nao wakija kwako, na kukuambia, Tufunulie sasa uliyomwambia mfalme; usimfiche, nasi hatutakuua; na pia uliyoambiwa na mfalme;
26. basi, utawaambia, Nalimwomba mfalme asinirudishe nyumbani kwa Yonathani, nisije nikafa humo.