1. Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, katika siku za Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, kusema,
2. Enenda nyumbani kwa Warekabi, ukanene nao, ukawalete nyumbani kwa BWANA, katika chumba kimoja, ukawape divai wanywe.
3. Basi nikamtwaa Yaazania, mwana wa Yeremia, mwana wa Habasinia, na ndugu zake, na wanawe wote, na nyumba yote ya Warekabi;
4. nikawaleta ndani ya nyumba ya BWANA, ndani ya chumba cha wana wa Hanani, mwana wa Igdalia, mtu wa Mungu, kilichokuwa karibu na chumba cha wakuu, nacho kilikuwa juu ya chumba cha Maaseya, mwana wa Shalumu, bawabu;
5. nikaweka mabakuli yaliyojaa divai, na vikombe, mbele ya wana wa nyumba ya Warekabi, nikawaambia, Nyweni divai.
6. Lakini wakasema, Hatutakunywa divai; kwa maana Yonadabu, mwana wa Rekabu, baba yetu, alituamuru, akisema, Msinywe divai, ninyi wala wana wenu, hata milele;
7. wala msijenge nyumba, wala msipande mbegu, wala msipande mizabibu, wala msiwe nayo; bali siku zenu zote mtakaa katika hema; mpate kuishi siku nyingi katika nchi ambayo mtakaa ndani yake hali ya wageni.
8. Nasi tumeitii sauti ya Yonadabu, mwana wa Rekabu, baba yetu, katika yote aliyotuamuru, kwamba tusinywe divai siku zetu zote, sisi, na wake zetu, na wana wetu, na binti zetu;
9. wala tusijijengee nyumba za kukaa; wala hatuna shamba la mizabibu, wala konde, wala mbegu;