1. Tena, neno la BWANA likamjia Yeremia mara ya pili, hapo alipokuwa akali amefungwa katika uwanda wa walinzi, kusema,
2. BWANA alitendaye jambo hili, BWANA aliumbaye ili alithibitishe; BWANA ndilo jina lake; asema hivi,
3. Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.
4. Maana BWANA, Mungu wa Israeli asema hivi, katika habari za nyumba za mji huu, na katika habari za nyumba za wafalme wa Yuda, zilizobomolewa ili kuyapinga maboma na upanga;
5. Wanakuja kupigana na Wakaldayo, lakini ni kuzijaza kwa mizoga ya watu, niliowaua katika hasira yangu na ghadhabu yangu, ambao kwa ajili ya uovu wao wote nimeuficha mji huu uso wangu.
6. Tazama, nitauletea afya na kupona, nami nitawaponya; nami nitawafunulia wingi wa amani na kweli.
7. Nami nitawarudisha wafungwa wa Yuda, na wafungwa wa Israeli, na kuwajenga kama kwanza.
8. Nami nitawasafisha na uovu wao wote, ambao kwa huo wamenitenda dhambi; nami nitawasamehe maovu yao yote, ambayo kwayo wamenitenda dhambi, na kukosa juu yangu.
9. Na mji huu utakuwa kwangu jina la furaha, na sifa na utukufu, mbele ya mataifa yote ya dunia, watakaosikia habari ya mema yote niwatendeayo, nao wataogopa na kutetemeka, kwa sababu ya mema yote na amani nitakaoupatia mji huo.
10. BWANA asema hivi, katika mahali hapo ambapo mnasema kwamba ni ukiwa, hapana mwanadamu wala mnyama, naam, katika miji ya Yuda na katika njia za Yerusalemu, zilizo ukiwa, hazina mwanadamu wala mwenyeji wala mnyama,
11. itasikilikana tena sauti ya furaha na sauti ya shangwe, sauti ya bwana arusi na sauti ya bibi arusi, sauti yao wasemao Mshukuruni BWANA wa majeshi, maana BWANA ni mwema, rehema zake ni za milele; na sauti zao waletao sadaka za shukrani nyumbani kwa BWANA. Kwa kuwa nitawarudisha wafungwa wa nchi hii kama kwanza, asema BWANA.
12. BWANA wa majeshi asema hivi, Katika mahali hapa, palipo ukiwa, hapana mwanadamu wala mnyama, na katika miji yake yote, yatakuwapo makao ya wachungaji wakizilaza kondoo zao.