2. Basi, wakati huo jeshi la mfalme wa Babeli liliuzunguka Yerusalemu; na Yeremia, nabii, alikuwa amefungwa ndani ya uwanda wa walinzi, uliokuwa katika nyumba ya mfalme wa Yuda.
3. Kwa maana Sedekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amemfunga, akisema, Kwa nini unatabiri, na kusema, BWANA asema hivi, Angalia, nitatia mji huu katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atautwaa;
4. tena, Sedekia, mfalme wa Yuda, hatapona kutoka katika mikono ya Wakaldayo, lakini hakika yake atatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli, atanena naye mdomo kwa mdomo, na macho yake yatatazama macho yake;
5. naye atamchukua Sedekia mpaka Babeli, naye atakuwako huko hata nitakapomjilia, asema BWANA; mjapopigana na Wakaldayo hamtafanikiwa.
6. Yeremia akasema, Neno la BWANA limenijia, kusema,
7. Tazama, Hanameli, mwana wa Shalumu, mjomba wako, atakujia, akisema, Jinunulie shamba langu lililoko Anathothi; maana haki ya ukombozi ni yako, ulinunue.
8. Basi Hanameli, mwana wa mjomba wangu, akanijia ndani ya uwanda wa walinzi, sawasawa na lile neno la BWANA, akaniambia, Tafadhali, ulinunue shamba langu lililoko Anathothi, katika nchi ya Benyamini; maana haki ya urithi ni yako, na haki ya ukombozi ni yako; ujinunulie. Ndipo nikajua kama neno hili ni neno la BWANA.
9. Basi nikalinunua shamba lile lililoko Anathothi kwa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, nikampimia fedha yake, shekeli kumi na saba za fedha.
10. Nami nikaitia sahihi ile hati, na kuipiga muhuri, nikawaita mashahidi, nikampimia ile fedha katika mizani.
11. Nikaitwaa ile hati ya kununua, ile iliyopigwa muhuri kama ilivyo sheria na ada, na ile nayo iliyokuwa wazi;