Yer. 31:29-40 Swahili Union Version (SUV)

29. Siku zile, hawatasema tena, Baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi.

30. Bali kila mtu atakufa kwa sababu ya uovu wake mwenyewe; kila mtu alaye zabibu kali, meno yake yatatiwa ganzi.

31. Angalia, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.

32. Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema BWANA.

33. Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema BWANA; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.

34. Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue BWANA; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema BWANA; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.

35. BWANA asema hivi, awapaye watu jua, ili kuwa nuru wakati wa mchana, na amri za mwezi na nyota, ili kuwa nuru wakati wa usiku, aichafuaye bahari, hata mawimbi yake yakavuma; BWANA wa majeshi, ndilo jina lake;

36. Amri hizi zikiondoka, zisiwe mbele zangu, asema BWANA, ndipo wazao wa Israeli nao wataacha kuwa taifa mbele zangu milele.

37. BWANA asema hivi, Kama mbingu zikiweza kupimwa, na misingi ya dunia ikiweza kugunduliwa huko chini, ndipo wazao wa Israeli pia nitawatupilia mbali, kwa ajili ya hayo yote waliyoyatenda, asema BWANA.

38. Tazama, siku zinakuja, asema BWANA, mji huu utakapojengwa kwa ajili ya BWANA, toka buruji ya Hananeli hata lango la pembeni.

39. Na kamba ya kupimia itaendelea moja kwa moja hata mlima Garebu, tena itazunguka na kufika Goa.

40. Na bonde lote la mizoga, na majivu, na mashamba yote mpaka kijito Kidroni, mpaka pembe ya lango la farasi, upande wa mashariki, patakuwa patakatifu kwa BWANA; hapatang’olewa, wala hapatabomolewa, hata milele.

Yer. 31