21. Jiwekee alama za njia; jifanyie miti ya kukuongoza; uuelekeze moyo wako kwenye njia kuu, njia ile ile uliyoiendea; rudi tena, Ee bikira wa Israeli, irudie hii miji yako.
22. Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume.
23. BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Watatumia tena neno hili katika nchi ya Yuda, na katika miji yake, nitakapowarudisha mateka yao; BWANA na akubariki, Ee kao la haki, Ee mlima wa utakatifu.
24. Na Yuda, na miji yake yote, watakaa humo pamoja; wakulima, nao waendao huko na huko pamoja na makundi yao.
25. Kwa maana nimeishibisha roho yenye uchovu, nami nimeiridhisha kila roho yenye huzuni.
26. Basi, nikaamka, nikaangalia; na usingizi wangu ulikuwa mtamu kwangu.
27. Tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapoipanda nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, mbegu ya mwanadamu na mbegu ya mnyama.
28. Tena itakuwa, kwa kadiri nilivyowaangalia, ili kung’oa, na kubomoa, na kuangusha, na kuangamiza, na kutesa; kwa kadiri iyo hiyo nitawaangalia, ili kujenga, na kupanda, asema BWANA.
29. Siku zile, hawatasema tena, Baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi.
30. Bali kila mtu atakufa kwa sababu ya uovu wake mwenyewe; kila mtu alaye zabibu kali, meno yake yatatiwa ganzi.