Yer. 30:10-21 Swahili Union Version (SUV)

10. Kwa sababu hiyo usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu, asema BWANA; wala usifadhaike, Ee Israeli; kwa maana, tazama, nitakuokoa toka mbali, na wazao wako toka nchi ya uhamisho wao; na Yakobo atarudi, naye atatulia na kustarehe, wala hapana mtu atakayemtia hofu.

11. Maana mimi ni pamoja nawe, asema BWANA, nikuokoe; maana nitawakomesha kabisa mataifa yote huko nilikokutawanya, bali sitakukomesha wewe kabisa; lakini nitakurudi kwa hukumu, wala sitakuacha bila adhabu.

12. Maana BWANA asema hivi, Maumivu yako hayaponyekani, na jeraha yako ni kubwa.

13. Hapana mtu wa kukutetea; kwa jeraha yako huna dawa ziponyazo.

14. Wote wakupendao wamekusahau; hawakutafuti; maana nimekujeruhi kwa jeraha ya adui, kwa adhabu ya mtu mkatili; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi zako zilikuwa zimeongezeka.

15. Mbona unalilia maumivu yako? Hayaponyeki maumivu yako; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi zako zimeongezeka, nimekutenda haya.

16. Basi, watu wote wakulao wataliwa; na adui zako wote watakwenda kufungwa; kila mmoja wao; na hao waliokuteka nyara watatekwa; na wote waliokuwinda nitawafanya kuwa mawindo.

17. Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema BWANA, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye.

18. BWANA asema hivi, Tazama, nitarudisha tena hema za Yakobo zilizohamishwa, na kuyahurumia makao yake; nao mji huo utajengwa juu ya magofu yake wenyewe, nalo jumba litakaliwa, kama ilivyokuwa desturi yake.

19. Tena kwao itasikiwa shukrani, na sauti yao wachangamkao; nami nitawazidisha, wala hawatakuwa wachache; tena nitawatukuza, wala hawatakuwa wanyonge.

20. Watoto wao nao watakuwa kama zamani, na kusanyiko lao litathibitika mbele zangu, nami nitawaadhibu wote wawaoneao.

21. Na mkuu wao atakuwa mtu wa kwao wenyewe, naye mwenye kuwatawala atakuwa mtu wa jamaa yao; nami nitamkaribisha, naye atanikaribia; maana ni nani aliye na moyo wa kuthubutu kunikaribia? Asema BWANA.

Yer. 30