Yer. 29:20-28 Swahili Union Version (SUV)

20. Basi, lisikieni neno la BWANA, ninyi nyote mliochukuliwa mateka, niliowapeleka toka Yerusalemu mpaka Babeli.

21. BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, katika habari za Ahabu, mwana wa Kolaya, na katika habari za Sedekia, mwana wa Maaseya, wawatabiriao ninyi maneno ya uongo kwa jina langu; Tazama, nitawatia katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, naye atawaua mbele ya macho yenu.

22. Tena katika habari zao laana itatumiwa na wafungwa wote wa Yuda, walioko Babeli, kusema, BWANA akufanye uwe kama Sedekia, na kama Ahabu, ambao mfalme wa Babeli aliwaoka motoni;

23. kwa sababu wametenda upumbavu katika Israeli, nao wamezini na wake za jirani zao, nao wamenena maneno ya uongo kwa jina langu, nisiyowaamuru; nami ndimi nijuaye, nami ni shahidi, asema BWANA.

24. Na katika habari za Shemaya, Mnehelami, utanena, ukisema,

25. BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, ya kwamba, Kwa kuwa kwa jina lako mwenyewe umewapelekea barua watu wote walioko Yerusalemu, na Sefania, mwana wa Maaseya, kuhani, na makuhani wote, kusema,

26. BWANA amekufanya kuhani badala ya Yehoyada, kuhani, ili mpate kuwa watumishi katika nyumba ya BWANA, kwa kila mtu aliye na wazimu, na kwa kila mtu ajifanyaye kuwa nabii, umtie katika mkatale na pingu.

27. Mbona, basi, hukumkemea Yeremia wa Anathothi, ajifanyaye kuwa nabii kwenu,

28. ambaye ametuma watu kwetu katika Babeli, kusema, Uhamisho huu ni wa siku nyingi; jengeni nyumba, mkakae ndani yake; pandeni bustani, mkale matunda yake.

Yer. 29