Yer. 27:2-16 Swahili Union Version (SUV)

2. BWANA ameniambia hivi, Jifanyizie vifungo na nira, ukajivike shingoni;

3. kisha uvipeleke kwa mfalme wa Edomu, na mfalme wa Moabu, na mfalme wa wana wa Amoni, na mfalme wa Tiro, na mfalme wa Sidoni, kwa mikono ya wajumbe watakaofika Yerusalemu kwa Sedekia, mfalme wa Yuda.

4. Uwaagize waende kwa bwana zao, na kuwaambia, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Mtawaambia bwana zenu maneno haya;

5. Mimi nimeiumba dunia hii, wanadamu na wanyama walio juu ya uso wa nchi, kwa uweza wangu mkuu, na kwa mkono wangu ulionyoshwa; nami nawapa watu kama inipendezavyo.

6. Na sasa nimetia nchi hizi zote katika mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu; na wanyama wa mwituni pia nimempa wamtumikie.

7. Na mataifa yote watamtumikia yeye, na mwanawe, na mwana wa mwanawe, hata utakapowadia wakati wa nchi yake mwenyewe, ndipo mataifa mengi na wafalme wakuu watamtumikisha yeye.

8. Na itakuwa, taifa lile na mfalme yule asiyetaka kumtumikia Nebukadreza, huyo mfalme wa Babeli, na kutia shingo zao katika nira ya mfalme wa Babeli, mimi nitaliadhibu taifa lile kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, asema BWANA, hata nitakapokuwa nimewaangamiza kwa mkono wake.

9. Lakini, katika habari zenu, msisikilize manabii wenu, wala wabashiri wenu, wala ndoto zenu, wala watambuzi wenu, wala waganga wenu, wanaowaambia, ya kwamba, Hamtamtumikia mfalme wa Babeli;

10. maana wanawatabiria uongo, ili kuwatoa ninyi mbali na nchi yenu; niwafukuze mkaangamie.

11. Bali taifa lile watakaotia shingo zao katika nira ya mfalme wa Babeli, na kumtumikia, taifa hilo nitawaacha wakae katika nchi yao wenyewe, asema BWANA; nao watailima, na kukaa ndani yake.

12. Nikamwambia Sedekia, mfalme wa Yuda, kwa mfano wa maneno hayo yote, nikisema, Tieni shingo zenu katika nira ya mfalme wa Babeli, mkamtumikie yeye na watu wake, mpate kuishi.

13. Mbona mnataka kufa, wewe na watu wako, kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, kama BWANA alivyosema katika habari ya taifa lile, lisilotaka kumtumikia mfalme wa Babeli?

14. Wala msisikilize maneno ya manabii wawaambiao ninyi, ya kwamba, Hamtamtumikia mfalme wa Babeli; maana wanawatabiria uongo.

15. Kwa maana mimi sikuwatuma, asema BWANA, bali wanatabiri uongo kwa jina langu; nipate kuwatoeni nje, mkaangamie, ninyi, na manabii hao wanaowatabiria.

16. Pia nalisema na makuhani, na watu wote, nikisema, BWANA asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wenu, wanaowatabiria, wakisema, Tazameni, vyombo vya nyumba ya BWANA, baada ya muda kidogo, vitaletwa tena toka Babeli; maana wanawatabiria uongo.

Yer. 27