Yer. 2:26-34 Swahili Union Version (SUV)

26. Kama mwivi aonavyo haya akamatwapo, ndivyo waonavyo haya nyumba ya Israeli; wao, na wafalme wao, na wakuu wao, na makuhani wao, na manabii wao;

27. waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana wamenipa mimi visogo, wala hawakunielekezea nyuso zao; lakini wakati wa taabu watasema, Simama ukatuokoe.

28. Lakini wako wapi miungu yako ulioifanya? Na wasimame hao, kama wakiweza kukuokoa wakati wa taabu yako; kwa maana hesabu ya miungu yako ni sawasawa na hesabu ya miji yako, Ee Yuda.

29. Mbona mnataka kuteta nami? Ninyi nyote mmeniasi, asema BWANA.

30. Nimewapiga watoto wako bure; hawakukubali kurudiwa; upanga wenu wenyewe umewala manabii wako, kama simba aharibuye.

31. Ee kizazi litazameni neno la BWANA. Je! Nimekuwa jangwa kwa Israeli? Au nchi yenye giza kuu? Mbona watu wangu wanasema, Sisi tumetoroka, hatutaki kuja kwako tena?

32. Je! Mwanamwali aweza kusahau mapambo yake, au bibi arusi mavazi yake? Lakini watu wangu wamenisahau mimi kwa muda wa siku zisizo na hesabu.

33. Jinsi ulivyoitengeneza njia yako ili kutafuta mapenzi! Kwa sababu hiyo hata wanawake wabaya umewafundisha njia zako.

34. Tena katika pindo za nguo zako imeonekana damu ya roho zao maskini wasio na hatia; sikuiona penye mahali palipobomoka, lakini naliiona juu ya hawa wote.

Yer. 2