19. Uovu wako mwenyewe utakurudi, maasi yako yatakukaripia; ujue, basi, ukaone, ya kuwa ni jambo baya sana na uchungu, kuwa umemwacha BWANA, Mungu wako, na ya kuwa moyoni mwako hamna kunihofu, asema Bwana, BWANA wa majeshi.
20. Kwa maana tangu zamani wewe umeivunja nira yako, na kuvipasua vifungo vyako; ukasema, Mimi sitatumika; kwa maana juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi, umejiinamisha, ukafanya mambo ya ukahaba.
21. Nami nalikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje, basi, kuwa mche usiofaa wa mzabibu-mwitu machoni pangu?
22. Maana ujapojiosha kwa magadi, na kujipatia sabuni nyingi, lakini uovu wako umeandikwa mbele zangu, asema Bwana MUNGU.
23. Wawezaje kusema, Sikutiwa unajisi, sikuwafuata Mabaali? Itazame njia yako bondeni, ujue uliyoyatenda; wewe u ngamia mwepesi, apitaye katika njia zake;
24. punda wa mwitu aliyeizoelea nyika, avutaye pumzi za upepo katika tamaa yake; katika wakati wake ni nani awezaye kumgeuza? Wote wamtafutao hawatajichokesha nafsi zao; katika mwezi wake watamwona.
25. Zuia mguu wako usikose kiatu, na koo yako isiwe na kiu; lakini wewe ulisema, Hapana matumaini kabisa; la, maana nimewapenda wageni, nami nitawafuata.
26. Kama mwivi aonavyo haya akamatwapo, ndivyo waonavyo haya nyumba ya Israeli; wao, na wafalme wao, na wakuu wao, na makuhani wao, na manabii wao;
27. waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana wamenipa mimi visogo, wala hawakunielekezea nyuso zao; lakini wakati wa taabu watasema, Simama ukatuokoe.
28. Lakini wako wapi miungu yako ulioifanya? Na wasimame hao, kama wakiweza kukuokoa wakati wa taabu yako; kwa maana hesabu ya miungu yako ni sawasawa na hesabu ya miji yako, Ee Yuda.
29. Mbona mnataka kuteta nami? Ninyi nyote mmeniasi, asema BWANA.
30. Nimewapiga watoto wako bure; hawakukubali kurudiwa; upanga wenu wenyewe umewala manabii wako, kama simba aharibuye.
31. Ee kizazi litazameni neno la BWANA. Je! Nimekuwa jangwa kwa Israeli? Au nchi yenye giza kuu? Mbona watu wangu wanasema, Sisi tumetoroka, hatutaki kuja kwako tena?