Yer. 2:1-11 Swahili Union Version (SUV)

1. Neno la BWANA likanijia, kusema,

2. Enenda ukalie masikioni mwa Yerusalemu, ukisema, BWANA asema hivi,Nakukumbuka, hisani ya ujana wako,upendo wa wakati wa uposo wako;Jinsi ulivyonifuata huko jangwani,katika nchi isiyopandwa mbegu.

3. Israeli walikuwa utakatifu kwa BWANA;malimbuko ya uzao wake;Wote watakaomla watakuwa na hatia;uovu utawajilia; asema BWANA.

4. Lisikieni neno la BWANA, ninyi nyumba ya Yakobo, na ninyi, jamaa zote za nyumba ya Israeli.

5. BWANA asema hivi, Baba zenu waliona dhuluma gani kwangu, hata wakafarakana nami, wakafuata ubatili, nao wakawa ubatili?

6. Wala hawakusema, Yuko wapi BWANA, aliyetutoa katika nchi ya Misri; akatuongoza jangwani, katika nchi ya ukame na mashimo, katika nchi ya kiu na ya kivuli cha mauti, katika nchi ambayo ndani yake hapiti mtu, wala haikukaliwa na watu?

7. Nami nikawatia katika nchi ya shibe, mpate kula matunda yake na mema yake; lakini ninyi mlipoingia katika nchi ile, mliitia unajisi nchi yangu, na urithi wangu mliufanya kuwa chukizo.

8. Makuhani hawakusema, Yuko wapi BWANA? Wala wana-sheria hawakunijua; wachungaji nao waliniasi, nao manabii walitoa unabii kwa Baali, wakafuata mambo yasiyofaidia kitu.

9. Basi, kwa ajili ya hayo nitateta nanyi, asema BWANA, nami nitateta na watoto wa watoto wenu.

10. Maana, vukeni mpaka visiwa vya Kitimu, mkaone; tumeni watu waende Kedari, mkafikiri sana; mkaone kwamba jambo kama hili limekuwa wakati wo wote.

11. Je! Taifa wamebadili miungu yao, ingawa siyo miungu? Lakini watu wangu wameubadili utukufu wao kwa ajili ya kitu kisichofaidia.

Yer. 2