6. Ee nyumba ya Israeli, je! Siwezi mimi kuwatendea ninyi vile vile kama mfinyanzi huyu alivyotenda? Asema BWANA. Angalieni, kama udongo ulivyo katika mkono wa mfinyanzi, ndivyo mlivyo ninyi katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli.
7. Wakati wo wote nitakapotoa habari za taifa, na habari za ufalme, kuung’oa, na kuuvunja, na kuuangamiza;
8. ikiwa taifa lile nililolitaja litageuka, na kuacha maovu yake nitaghairi, nisitende mabaya yale niliyoazimia kuwatenda.
9. Na wakati wo wote nitakapotoa habari za taifa, na habari za ufalme, kuujenga na kuupanda,
10. ikiwa watatenda maovu mbele za macho yangu, wasiitii sauti yangu, basi nitaghairi, nisitende mema yale niliyoazimia kuwatendea.
11. Haya! Basi, ukawaambie watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, ukisema, BWANA asema hivi, Tazama, ninafinyanga mabaya juu yenu, na kuwaza mawazo juu yenu; rudini sasa, kila mmoja na aiache njia yake mbaya; zitengenezeni njia zenu, na matendo yenu.
12. Lakini wao wasema, Hapana tumaini lo lote; maana sisi tutafuata mawazo yetu wenyewe, nasi tutatenda kila mmoja wetu kwa kuufuata ushupavu wa moyo wake mbaya.
13. Basi, kwa ajili ya hayo, BWANA asema hivi, Ulizeni sasa katika mataifa, ni nani aliyesikia habari za mambo kama hayo; bikira wa Israeli ametenda tendo lichukizalo sana.
14. Je! Theluji ya Lebanoni itakoma katika jabali la kondeni? Au je! Maji ya baridi yashukayo toka mbali yatakauka?
15. Maana watu wangu wamenisahau, wameufukizia ubatili uvumba; nao wamewakaza katika njia zao, katika mapito ya zamani, ili wapite katika njia za kando, katika njia isiyotengenezwa;
16. ili kufanya nchi yao kuwa kitu cha kushangaza, na cha kuzomewa daima; kila mtu apitaye karibu nayo atashangaa, na kutikisa kichwa chake.
17. Nami nitawatawanya mbele ya adui, kama kwa upepo wa mashariki; nami nitaviangalia visogo vyao, wala si nyuso zao, siku ya msiba wao.