1. BWANA akaniambia hivi, Enenda, ukajinunulie mshipi wa kitani, ukajivike viuno, wala usiutie majini.
2. Basi nikanunua mshipi sawasawa na neno la BWANA, nikajivika viunoni.
3. Nalo neno la BWANA likanijia mara ya pili, kusema,
4. Twaa mshipi ule ulioununua, ulio viunoni mwako, kisha ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukaufiche huko katika pango la jabali.
5. Basi nikaenda, nikauficha karibu na mto Frati, kama BWANA alivyoniamuru.
6. Hata ikawa, baada ya siku nyingi, BWANA akaniambia, Ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukautwae ule mshipi, niliokuamuru kuuficha huko.
7. Ndipo nikaenda mpaka mto Frati, nikachimba, nikautwaa ule mshipi katika mahali pale nilipouficha; na tazama, mshipi ulikuwa umeharibika, haukufaa tena kwa lo lote.
8. Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema,
9. BWANA asema hivi, Jinsi iyo hiyo nitakiharibu kiburi cha Yuda, na kiburi kikuu cha Yerusalemu.
10. Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wanaokwenda kwa ushupavu wa mioyo yao, na kufuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu, watakuwa hali moja na mshipi huu, usiofaa kwa lo lote.
11. Maana kama vile mshipi unavyoshikamana na viuno vya mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami nyumba yote ya Israeli; na nyumba yote ya Yuda, asema BWANA; wapate kuwa watu kwangu mimi, na jina, na sifa, na utukufu; lakini hawakutaka kusikia.
12. Basi utawaambia neno hili, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kila chupa itajazwa divai; nao watakuambia, Je, sisi hatujui ya kuwa kila chupa itajazwa divai?
13. Ndipo utakapowaambia, BWANA asema hivi, Tazama, nitawajaza ulevi wenyeji wote wa nchi hii, hata wafalme wanaoketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na makuhani, na manabii, na wenyeji wote wa Yerusalemu.