Yer. 11:12-20 Swahili Union Version (SUV)

12. Ndipo miji ya Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, watakwenda na kuwalilia miungu wawafukiziao uvumba; lakini hawatawaokoa hata kidogo wakati wa taabu yao.

13. Maana hesabu ya miungu yako, Ee Yuda, ni sawasawa na hesabu ya miji yako; na kama ilivyo hesabu ya njia za Yerusalemu, ndivyo mlivyosimamisha madhabahu za kitu kile cha aibu, madhabahu za kumfukizia Baali uvumba.

14. Basi, usiwaombee watu hawa, wala usipaze sauti yako, wala kuwaombea dua watu hawa; maana sitawasikia wakati watakaponililia kwa ajili ya taabu yao.

15. Mpenzi wangu afanya nini nyumbani mwangu, ikiwa amefanya uasherati? Je! Nadhiri zako na nyama takatifu zitakuondolea hatia? Ufanyapo maovu, ndipo uonapo furaha.

16. BWANA alikuita jina lako, Mzeituni wenye majani mabichi, mzuri, wenye matunda mema; kwa kelele za mshindo mkuu amewasha moto juu yake, na matawi yake yamevunjika.

17. Kwa maana BWANA wa majeshi, aliyekupanda, ametamka mabaya juu yako, kwa sababu ya maovu ya nyumba ya Israeli, na ya nyumba ya Yuda, waliyoyatenda juu ya nafsi zao wenyewe kwa kunikasirisha, wakimfukizia Baali uvumba.

18. Tena BWANA akanijulisha haya, nami nikayajua; ndipo uliponionyesha matendo yao.

19. Lakini mimi nalikuwa kama mwana-kondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa; wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena.

20. Lakini, Ee BWANA wa majeshi, uhukumuye haki, ujaribuye viuno na moyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.

Yer. 11