Yer. 11:1-10 Swahili Union Version (SUV)

1. Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema,

2. Yasikieni maneno ya maagano haya; ukaseme na watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu;

3. ukawaambie, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Na alaaniwe mtu asiyeyasikia maneno ya maagano haya,

4. niliyowaamuru baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, katika tanuru ya chuma, nikisema, Itiini sauti yangu, mkafanye sawasawa na yote niwaagizayo ninyi; ndivyo mtakavyokuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu;

5. ili nipate kukitimiza kiapo nilichowaapia baba zenu, kuwapa nchi ijaayo maziwa na asali, kama ilivyo leo hivi. Ndipo nikajibu, nikasema, Amina, Ee BWANA.

6. Naye BWANA akaniambia, Hubiri maneno haya yote katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, ukisema, Yasikieni maneno ya maagano haya, mkayafanye.

7. Kwa maana naliwashuhudia sana baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, hata leo, nikiamka mapema na kuwashuhudia, nikisema, Itiini sauti yangu.

8. Lakini hawakutii, wala kutega masikio yao, bali walikwenda kila mtu katika ushupavu wa moyo wake mbaya; kwa hiyo nimeleta juu yao maneno yote ya maagano haya, niliyowaamuru wayafanye; lakini hawakuyafanya.

9. Naye BWANA akaniambia, Fitina imeonekana katika watu wa Yuda, na katika wenyeji wa Yerusalemu.

10. Wameyarudia maovu ya baba zao, waliokataa kusikia maneno yangu; wamewafuata miungu mingine na kuwatumikia; nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, wameyavunja maagano yangu niliyoyafanya na baba zao.

Yer. 11