8. Kisha mwingine, malaika wa pili, akafuata, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake.
9. Na mwingine, malaika wa tatu, akawafuata, akisema kwa sauti kuu, Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake,
10. yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake; naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-Kondoo.
11. Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku, hao wamsujuduo huyo mnyama na sanamu yake, na kila aipokeaye chapa ya jina lake.
12. Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.