10. Mambo hayo yatawapata kwa sababu ya kiburi chao, kwa kuwa wamewatukana watu wa BWANA wa majeshi, na kujitukuza juu yao.
11. BWANA atakuwa mwenye kuwatisha sana; kwa maana atawafisha kwa njaa miungu yote ya dunia; na watu watamsujudia yeye, kila mtu toka mahali pake; naam, nchi zote za mataifa.
12. Na ninyi Wakushi pia, mtauawa kwa upanga wangu.
13. Naye atanyosha mkono wake juu ya upande wa kaskazini, na kuiangamiza Ashuru; naye ataufanya Ninawi kuwa ukiwa, kuwa mahali pakavu kama jangwa.
14. Na makundi ya wanyama watalala kati yake, wanyama wote wa mataifa; mwari-nyuni na nungu watakaa juu ya vichwa vya nguzo zake; sauti yao itasikiwa madirishani; vizingitini mwake mtakuwa ukiwa; kwa maana ameifunua kazi ya mierezi.