Rut. 1:4-15 Swahili Union Version (SUV)

4. Nao wakaoa wake katika wanawake wa Moabu; na jina la mmoja aliitwa Orpa, na jina la wa pili Ruthu. Wakakaa huko yapata miaka kumi.

5. Wakafa na Maloni na Kilioni wote wawili; na huyo mwanamke akawa amefiwa na wanawe wawili, na mumewe pia.

6. Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana huko katika nchi ya Moabu amesikia ya kwamba BWANA amewajilia watu wake na kuwapa chakula.

7. Basi akatoka pale alipokuwapo, na wakweze wawili pamoja naye; wakashika njia ili kurudi mpaka nchi ya Yuda.

8. Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; BWANA na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia.

9. BWANA na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao wakalia.

10. Wakamwambia, La, sivyo; lakini tutarudi pamoja nawe kwa watu wako.

11. Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, mrejee; kwani kufuatana na mimi? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu?

12. Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume;

13. je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa BWANA umetoka juu yangu.

14. Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye.

15. Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako.

Rut. 1