Rum. 9:17-31 Swahili Union Version (SUV)

17. Kwa maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.

18. Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu, na atakaye kumfanya mgumu humfanya mgumu.

19. Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake?

20. La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi?

21. Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?

22. Ni nini basi, ikiwa Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake, na kuudhihirisha uweza wake, kwa uvumilivu mwingi, alichukuliana na vile vyombo vya ghadhabu vilivyofanywa tayari kwa uharibifu;

23. tena, ili audhihirishe wingi wa utukufu wake katika vile vyombo vya rehema, alivyovitengeneza tangu zamani vipate utukufu;

24. ndio sisi aliotuita, si watu wa Wayahudi tu, ila na watu wa Mataifa pia?

25. Ni kama vile alivyosema katika Hosea,Nitawaita watu wangu wale wasiokuwa watu wangu,Na mpenzi wangu yeye asiyekuwa mpenzi wangu.

26. Tena itakuwa mahali pale walipoambiwa,Ninyi si watu wangu,Hapo wataitwa wana wa Mungu aliye hai.

27. Isaya naye atoa sauti yake juu ya Israeli, kusema,Hesabu ya wana wa Israeli, ijapokuwa ni kama mchanga wa bahari, ni mabaki yao tu watakaookolewa.

28. Kwa maana Bwana atalitekeleza neno lake juu ya nchi, akilimaliza na kulikata.

29. Tena kama Isaya alivyotangulia kunena,Kama Bwana wa majeshi asingalituachia uzao,Tungalikuwa kama Sodoma, tungalifananishwa na Gomora.

30. Tuseme nini, basi? Ya kwamba watu wa Mataifa, wasioifuata haki, walipata haki; lakini ni ile haki iliyo ya imani;

31. bali Israeli wakiifuata sheria ya haki hawakuifikilia ile sheria.

Rum. 9