9. Na mashujaa wako, Ee Temani, watafadhaika, hata iwe kila mtu akatiliwe mbali kwa kuuawa katika kilima cha Esau.
10. Kwa sababu ya udhalimu aliotendwa ndugu yako Yakobo, aibu itakufunika, nawe utakatiliwa mbali hata milele.
11. Siku ile uliposimama upande, siku ile wageni walipochukua mali zake, na watu wa kabila nyingine walipoingia katika malango yake, na kumpa kura juu ya Yerusalemu, wewe nawe ulikuwa kama mmoja wao.
12. Lakini usiitazame siku ya ndugu yako, siku ya mashaka yake, wala usisimange juu ya wana wa Yuda siku ya kuangamizwa kwao; wala usinene maneno ya kiburi katika siku ya shida yao.
13. Usiingie katika lango la watu wangu, siku ya msiba wao; naam, usiyatazame mateso yao, siku ya msiba wao; wala usitie mikono yako juu ya mali zao, siku ya msiba wao.
14. Wala usisimame penye njia panda, ili kuwakatilia mbali watu wake wakimbiao; wala usiwatoe watu wake waliosalia, katika siku ya dhiki.
15. Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe.
16. Kwa maana kama vile mlivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu, ndivyo mataifa yote watakavyokunywa daima; naam, watakunywa na kubabaika, nao watakuwa kana kwamba hawakuwa kamwe.
17. Bali katika mlima Sayuni watakuwako wenye kuokoka, nao utakuwa mtakatifu; na nyumba ya Yakobo watamiliki milki zao.
18. Na nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yusufu itakuwa mwali wa moto, na nyumba ya Esau itakuwa mabua makavu, nao watawaka kati yao, na kuwateketeza; wala hatasalia mtu awaye yote katika nyumba ya Esau; kwa kuwa BWANA amesema hayo.