6. Mfalme akaniuliza, (malkia naye ameketi karibu naye), Safari yako itakuwa ya siku ngapi? Nawe utarudi lini? Hivyo mfalme akaona vema kunipeleka; nami nikampa muda.
7. Tena nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na nipewe nyaraka kwa maliwali walio ng’ambo ya Mto, ili waniache kupita mpaka nifike Yuda;
8. nipewe na waraka kwa Asafu, mwenye kuutunza mwitu wa mfalme, ili anipe miti ya kufanyizia boriti kwa malango ya ngome ya nyumba, na kwa ukuta wa mji; na kwa nyumba ile nitakayoingia mimi. Naye mfalme akanipa, kama mkono mwema wa Mungu wangu ulivyokuwa juu yangu.
9. Ndipo nikafika kwa maliwali walio ng’ambo ya Mto, nikawapa hizo nyaraka za mfalme. Naye mfalme alikuwa amepeleka maakida wa jeshi lake na wapanda farasi pamoja nami.
10. Hata Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, mtumishi wake, Mwamoni, waliposikia habari hizi, ziliwahuzunisha sana, kwa kuwa amekuja mtu kuwatakia heri wana wa Israeli.
11. Basi nikafika Yerusalemu, nikakaa huko muda wa siku tatu.
12. Kisha nikaondoka usiku, mimi na watu wachache pamoja nami; wala sikumwambia mtu neno hili alilolitia Mungu wangu moyoni mwangu, nilitende kwa ajili ya Yerusalemu; wala hapakuwa na mnyama pamoja nami, ila mnyama yule niliyempanda mwenyewe.
13. Nikatoka nje usiku, kwa njia ya lango la bondeni, nikashika njia iendayo kisima cha joka, na lango la jaa; nikazitazama kuta za Yerusalemu, zilizokuwa zimebomoka; na malango yake yameteketezwa kwa moto.
14. Kisha nikaendelea mpaka lango la chemchemi, na ziwa la mfalme; lakini hapakuwa na nafasi ya kupita kwa yule mnyama aliyekuwa chini yangu.