Neh. 13:1-14 Swahili Union Version (SUV)

1. Siku hiyo walisoma katika kitabu cha Musa masikioni mwa watu; na ndani yake yalionekana maneno haya yameandikwa, ya kwamba Mwamoni na Mmoabi wasiingie katika kusanyiko la Mungu milele;

2. kwa sababu hawakuwalaki wana wa Israeli kwa chakula na maji, bali walimwajiri Balaamu juu yao ili awalaani; lakini Mungu aliigeuza ile laana kuwa baraka.

3. Ikawa walipoisikia torati, wakawatenga Israeli na umati wa watu waliochanganyika nao.

4. Na kabla ya hayo, Eliashibu, kuhani, aliyewekwa avisimamie vyumba vya nyumba ya Mungu wetu, kwa kuwa alikuwa karibu yake Tobia,

5. alikuwa amemtengenezea chumba kikubwa, hapo walipoweka zamani sadaka za unga, na ubani, na vyombo, na zaka za nafaka, na divai, na mafuta, walivyoamriwa kuwapa Walawi, na waimbaji, na mabawabu; tena sadaka za kuinuliwa zilizokuwa za makuhani.

6. Lakini wakati huo wote mimi sikuwako huko Yerusalemu; maana katika mwaka wa thelathini na mbili wa Artashasta, mfalme wa Babeli, nalimrudia mfalme; na baada ya siku kadha wa kadha nikaomba ruhusa tena kwa mfalme.

7. Nami nikaja Yerusalemu, nikafahamu yale mabaya, ambayo Eliashibu ameyatenda kwa ajili ya Tobia, kwa kumtengenezea chumba katika nyua za nyumba ya Mungu.

8. Nami nikasikitika sana; basi nikavitupa nje vyombo vyote vya Tobia vitoke humo chumbani.

9. Kisha nikatoa amri, nao wakavisafisha vyumba; nami nikavirudisha humo vyombo vya nyumba ya Mungu, pamoja na sadaka za unga na ubani.

10. Tena nikaona ya kwamba Walawi hawakupewa sehemu zao; basi wamekimbia Walawi na waimbaji, waliofanya kazi, kila mtu shambani kwake.

11. Ndipo nikagombana na mashehe, nikasema, Mbona nyumba ya Mungu imeachwa? Kisha nikawakusanya, nikawaweka mahali pao.

12. Ndipo Yuda wote walipoleta zaka za nafaka, na mvinyo, na mafuta, kwenye hazina.

13. Nami nikawaweka watunza hazina juu ya hazina, yaani, Shelemia kuhani, na Sadoki mwandishi, na wa Walawi, Pedaya; na wa pili wao alikuwa Hanani, mwana wa Zakuri, mwana wa Matania; kwani walihesabiwa kuwa waaminifu, na ilikuwa juu yao kuwagawia ndugu zao.

14. Unikumbukie hayo, Ee Mungu wangu, wala usifute fadhili zangu nilizozitenda kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu, na kwa taratibu zake.

Neh. 13