1. Ole wake mji wa damu! Umejaa mambo ya uongo na unyang’anyi; mateka hayaondoki.
2. Kelele za mjeledi, kelele za magurudumu yafanyayo kishindo; na farasi wenye kupara-para, na magari ya vita yenye kuruka-ruka;
3. mpanda farasi akipanda, na upanga ukimeta-meta, na mkuki ukimemetuka; na wingi wa waliouawa, na chungu kubwa ya mizoga; mizoga haina mwisho; wanajikwaa juu ya mizoga yao.
4. Kwa sababu ya wingi wa ukahaba wa yule kahaba mzuri, yule bibi wa mambo ya uchawi, auzaye mataifa kwa ukahaba wake, na jamaa za watu kwa uchawi wake.
5. Tazama, mimi ni juu yako, asema BWANA wa majeshi; nami nitafunua marinda yako mbele ya uso wako; nami nitawaonyesha mataifa uchi wako, na falme aibu yako.
6. Nami nitatupa uchafu uchukizao juu yako, kukufanya uwe mchafu, nami nitakufanya kuwa kitu cha kutazamwa kwa dharau.
7. Hata itakuwa, wote wakutazamao watakukimbia, wakisema, Ninawi umeharibika; ni nani atakayeuhurumia? Nikutafutie wapi wafariji?
8. Je! Wewe u mwema kuliko No-amoni, uliowekwa kati ya mito, uliozungukwa na maji; ambao boma lake lilikuwa bahari, na bahari ilikuwa ukuta wake.