Mwa. 9:14-28 Swahili Union Version (SUV)

14. Hata itakuwa nikitanda mawingu juu ya nchi, upinde utaonekana winguni,

15. nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili.

16. Basi huo upinde utakuwa winguni; nami nitauangalia nipate kulikumbuka agano la milele lililoko kati ya Mungu na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili kilichoko katika nchi.

17. Mungu akamwambia Nuhu, Hii ndiyo ishara ya agano nililoliweka kati yangu na wote wenye mwili walioko katika nchi.

18. Wana wa Nuhu waliotoka katika safina, ni Shemu, na Hamu, na Yafethi; na Hamu ndiye baba wa Kanaani.

19. Hawa watatu walikuwa wana wa Nuhu na kwa hao nchi yote ikaenea watu.

20. Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu;

21. akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake.

22. Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje.

23. Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao; na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao.

24. Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea.

25. Akasema,Na alaaniwe Kanaani;Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake.

26. Akasema,Na atukuzwe BWANA Mungu wa Shemu;Na Kanaani awe mtumwa wake.

27. Mungu akamnafisishe Yafethi.Na akae katika hema za Shemu;Na Kanaani awe mtumwa wake.

28. Na Nuhu akaishi baada ya ile gharika miaka mia tatu na hamsini.

Mwa. 9