Mwa. 50:11-26 Swahili Union Version (SUV)

11. Nao waliokaa katika nchi, wale Wakanaani, walipoyaona matanga katika sakafu ya Atadi, wakasema, Matanga haya ya Wamisri ni makuu kwa hiyo mahali pale paliitwa Abel-Misri, iliyo ng’ambo ya Yordani.

12. Wanawe wakamfanyia kama alivyo waagiza;

13. kwa kuwa wanawe wakamchukuwa mpaka nchi ya Kanaani, nao wakamzika katika pango ya shamba la Makpela, iliyo mbele ya Mamre, aliyoinunua Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake pa kuzikia.

14. Yusufu akarudi Misri, yeye na ndugu zake, na wote waliyokwenda pamoja naye kumzika babaye, baada ya kumzika babaye.

15. Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda.

16. Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema,

17. Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye.

18. Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako.

19. Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu?

20. Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.

21. Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema.

22. Akakaa Yusufu katika Misri, yeye na nyumba ya babaye. Akaishi Yusufu miaka mia na kumi.

23. Yusufu akaona wana wa Efraimu hata kizazi cha tatu; na wana wa Makiri, mwana wa Manase, walizaliwa magotini mwa Yusufu.

24. Yusufu akawaambia nduguze, Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.

25. Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akasema, Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu.

26. Basi Yusufu akafa, mwenye miaka mia na kumi; wakampaka dawa, wakamtia katika sanduku, huko Misri.

Mwa. 50