Mwa. 49:21-33 Swahili Union Version (SUV)

21. Naftali ni ayala aliyefunguliwa;Anatoa maneno mazuri.

22. Yusufu ni mti mchanga wenye kuzaa,Mti mchanga wenye kuzaa karibu na chemchemi,Matwi yake yametanda ukutani.

23. Wapiga mishale walimtenda machungu,Wakamtupia, wakamwudhi,

24. Lakini upinde wake ukakaa imara,Mikono yake ikapata nguvu,Kwa mikono ya Mwenye Enzi wa Yakobo;Kwa jina la mchungaji, yeye jiwe la Israeli,

25. Naam, kwa Mungu wa baba yako atakaye kusaidia;Kwa mibaraka ya mbinguni juu.Mibaraka ya vilindi vilivyo chini,Mibaraka ya maziwa, na ya mimba.

26. Mibaraka ya baba yakoImepita mibaraka ya milima ya kale,Vitu vinavyotamanika vya vilima vya milele;Na vikae juu ya kichwa cha Yusufu,Juu ya utosi wa kichwa chake aliye mkuu kati ya ndugu zake.

27. Benyamini ni mbwa-mwitu mwenye kurarua-raruaAsubuhi atakula mawindo,Na jioni atagawanya mateka.

28. Hizo zote ndizo kabila za Israeli kumi na mbili. Na hayo ndiyo aliyowaambia baba yao, na kuwabariki; mmoja mmoja kwa mbaraka wake aliwabariki.

29. Akawaamuru, akasema, Mimi ninakwenda kukusanywa pamoja na watu wangu; mnizike pamoja na baba zangu, katika pango iliyomo shambani mwa Efroni, Mhiti;

30. katika ile pango iliyomo shambani mwa Makpela, iliyo mbele ya Mamre katika nchi ya Kanaani, aliyoinunua Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake ya kuzikia.

31. Humo walimzika Ibrahimu, na Sara mkewe; humo wakamzika Isaka, na Rebeka mkewe; nami humo nikamzika Lea;

32. shamba na pango iliyomo lililonunuliwa kwa wazawa wa Hethi.

33. Basi Yakobo alipokwisha kuwaagiza wanawe, akakunja miguu yake kitandani, akafa, akakusanywa pamoja na watu wake.

Mwa. 49