Mwa. 47:7-18 Swahili Union Version (SUV)

7. Yusufu akamleta Yakobo babaye ndani akamweka mbele ya Farao Yakobo akambariki Farao.

8. Farao akamwuliza Yakobo, Je! Siku za miaka ya maisha yako ni ngapi?

9. Yakobo akamjibu Farao, Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu, wala hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya baba zangu katika siku za kusafiri kwao.

10. Yakobo akambariki Farao, akatoka mbele ya Farao.

11. Yusufu akawakalisha babaye na nduguze, na kuwapa milki katika nchi ya Misri, katika mahali pazuri pa nchi, katika nchi ya Ramesesi, kama Farao alivyoamuru.

12. Naye Yusufu akawalisha babaye na nduguze na nyumba yote ya babaye, kwa kadiri ya hesabu ya watoto wao.

13. Wala hapakuwa na chakula katika nchi yote, kwa kuwa njaa ilikuwa nzito sana, hata nchi ya Misri, na nchi ya Kanaani zikataabika, kwa sababu ya njaa.

14. Yusufu akakusanya fedha zote zilizoonekana katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, kwa nafaka waliyoinunua. Yusufu akazileta zile fedha nyumbani mwa Farao.

15. Fedha zote zilipokwisha katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, Wamisri wote walimjia Yusufu, wakisema, Tupe sisi chakula, kwa nini tufe mbele ya macho yako? Maana fedha zetu zimekwisha.

16. Yusufu akasema, Toeni wanyama wenu, nami nitawapa chakula badala ya wanyama wenu, kama fedha zenu zimekwisha.

17. Wakaleta wanyama wao kwa Yusufu; Yusufu akawapa chakula badala ya farasi, na badala ya kondoo, na badala ya ng’ombe, na badala ya punda, naye akawalisha chakula badala ya wanyama wao wote mwaka ule.

18. Na mwaka ule ulipokwisha wakamjia mwaka wa pili, wakamwambia, Hatumfichi bwana wetu ya kwamba fedha zetu zimekwisha, na makundi ya wanyama ni mali ya bwana wetu, hakikusalia kitu mbele ya bwana wetu, ila miili yetu na nchi zetu.

Mwa. 47