1. Ikawa, baada ya mambo hayo, mnyweshaji wa mfalme wa Misri, na mwokaji wake, wakamkosa bwana wao, mfalme wa Misri.
2. Farao akawaghadhibikia maakida wake wawili, mkuu wa wanyweshaji na mkuu wa waokaji.
3. Akawatia katika lindo nyumbani mwa mkuu wa askari, humo gerezani, mahali alipofungwa Yusufu.
4. Mkuu wa askari akamwekea Yusufu watu hao, naye akawahudumu, nao wakakaa siku kadha wa kadha katika kifungo.
5. Wakaota ndoto wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliofungwa gerezani.
6. Yusufu akawajia asubuhi, akawaona wamefadhaika.
7. Akawauliza hao maakida wa Farao, waliokuwa pamoja naye katika kifungo, nyumbani mwa bwana wake, akisema, Mbona nyuso zenu zimekunjamana leo?
8. Wakamwambia, Tumeota ndoto wala hapana awezaye kuifasiri. Yusufu akawaambia, Kufasiri si kazi ya Mungu? Tafadhalini mniambie.