16. Kaini akatoka mbele za uso wa BWANA, akakaa katika nchi ya Nodi, mbele ya Edeni.
17. Kaini akamjua mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Henoko; akajenga mji akauita Henoko, kwa jina la mwanawe.
18. Henoko akamzaa Iradi, Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli; Methushaeli akamzaa Lameki.
19. Lameki akajitwalia wake wawili, jina la wa kwanza ni Ada, na jina la wa pili ni Sila.
20. Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama.
21. Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi.
22. Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake Tubal-kaini alikuwa Naama.
23. Lameki akawaambia wake zake,Sikieni sauti yangu, Ada na Sila;Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu;Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha;Kijana kwa kunichubua;
24. Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba,Hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba.
25. Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua.
26. Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la BWANA.