Mwa. 38:5-19 Swahili Union Version (SUV)

5. Akaendelea, akazaa tena mwana mwingine, akamwita jina lake Shela. Naye Yuda alikuwako huko Kezibu, alipomzaa.

6. Yuda akamwoza mke Eri, mzaliwa wake wa kwanza, na jina lake huyo mke ni Tamari.

7. Naye Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mbaya machoni pa BWANA; na BWANA akamwua.

8. Yuda akamwambia Onani, Uingie kwa mke wa nduguyo, ukamwoe, ukamwinulie nduguyo uzao.

9. Onani alijua ya kwamba huo uzao hautakuwa wake, ikawa, alipoingia kwa mke wa nduguye, akamwagia chini asimpe nduguye uzao.

10. Neno hili alilolifanya likawa baya machoni pa BWANA, basi akamwua yeye naye.

11. Yuda akamwambia Tamari mkwewe, Ukae mjane nyumbani mwa baba yako hata Shela mwanangu atakapokuwa mtu mzima, maana alisema, Asipate kufa yeye kama nduguze. Basi Tamari akaenda, akakaa nyumbani mwa babaye.

12. Siku nyingi zikapita, akafa binti Shua, mkewe Yuda. Yuda akafarijika, akaenda kwa watu wake wawakatao manyoya kondoo huko Timna, yeye na mwenzake Hira, Mwadulami.

13. Huyo Tamari akapewa habari, kusema, Mkweo anakwenda Timna, akate manyoya ya kondoo zake.

14. Basi akavua nguo za ujane wake, akajivika utaji, akajifunika uso, akakaa mlangoni pa Enaimu, karibu na njia ya kuendea Timna. Maana aliona ya kwamba Shela amekuwa mtu mzima, wala hakuozwa awe mkewe.

15. Yuda alipomwona alimdhania kuwa ni kahaba, maana amejifunika uso.

16. Akamgeukia kando ya njia, akasema, Niruhusu niingie kwako. Maana hakujua ya kuwa ni mkwewe. Akamwuliza, Utanipa nini, ukiingia kwangu?

17. Akasema, Nitakuletea mwana-mbuzi wa kundini. Naye akamwuliza, Je! Utanipa rehani hata utakapomleta?

18. Akasema, Nikupe rehani gani? Akamjibu, Pete yako ya muhuri, na kamba yake, na fimbo yako iliyo mkononi mwako. Basi akampa, akaingia kwake, naye akapata mimba.

19. Akaondoka, akaenda zake, akavua utaji wake, na kuvaa mavazi ya ujane wake.

Mwa. 38