14. Basi akavua nguo za ujane wake, akajivika utaji, akajifunika uso, akakaa mlangoni pa Enaimu, karibu na njia ya kuendea Timna. Maana aliona ya kwamba Shela amekuwa mtu mzima, wala hakuozwa awe mkewe.
15. Yuda alipomwona alimdhania kuwa ni kahaba, maana amejifunika uso.
16. Akamgeukia kando ya njia, akasema, Niruhusu niingie kwako. Maana hakujua ya kuwa ni mkwewe. Akamwuliza, Utanipa nini, ukiingia kwangu?
17. Akasema, Nitakuletea mwana-mbuzi wa kundini. Naye akamwuliza, Je! Utanipa rehani hata utakapomleta?
18. Akasema, Nikupe rehani gani? Akamjibu, Pete yako ya muhuri, na kamba yake, na fimbo yako iliyo mkononi mwako. Basi akampa, akaingia kwake, naye akapata mimba.
19. Akaondoka, akaenda zake, akavua utaji wake, na kuvaa mavazi ya ujane wake.
20. Yuda akapeleka yule mwana-mbuzi kwa mkono wa rafiki yake Mwadulami, ili aipate rehani mkononi mwa huyo mwanamke lakini hakumkuta.
21. Akauliza watu wa mahali pale, akisema, Yuko wapi yule kahaba aliyekuwapo Enaimu kando ya njia? Wakasema, Hakuwako hapa kahaba.
22. Akamrudia Yuda akasema, Sikumwona; hata na watu wa mahali hapo walisema, Hakuwako kahaba.