6. akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota.
7. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu.
8. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake.
9. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia.
10. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi?
11. Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.
12. Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu.
13. Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao. Akamwambia, Mimi hapa.
14. Akamwambia, Enenda, basi, ukaone kama ndugu zako hawajambo, na kundi nalo li salama, ukaniletee habari. Basi akampeleka kutoka bonde la Hebroni, akafika Shekemu.
15. Mtu mmoja akamkuta, naye alikuwa anazunguka-zunguka katika nyika; yule mtu akamwuliza, akisema, Unatafuta nini?
16. Akasema, Nawatafuta ndugu zangu; tafadhali uniambie mahali wanakochunga.
17. Yule mtu akasema, Wametoka hapa, maana niliwasikia wakisema, Twendeni Dothani. Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani.