Mwa. 37:3-12 Swahili Union Version (SUV)

3. Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu.

4. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani.

5. Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia;

6. akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota.

7. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu.

8. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake.

9. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia.

10. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi?

11. Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.

12. Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu.

Mwa. 37