Mwa. 34:5-17 Swahili Union Version (SUV)

5. Basi Yakobo akasikia ya kwamba amembikiri Dina, binti yake. Na wanawe walikuwako pamoja na wanyama wake nyikani. Yakobo akanyamaza, hata walipokuja.

6. Akatoka Hamori, babaye Shekemu, kumwendea Yakobo, aseme naye.

7. Wanawe Yakobo waliposikia hayo, wakaja kutoka nyikani; nao wakasikitika sana, wakakasirika mno, kwa sababu amefanya upumbavu katika Israeli kwa kulala na binti Yakobo, neno lisilojuzu kutendeka.

8. Hamori akasema nao, akinena, Roho ya Shekemu, mwanangu, inamtamani binti yenu, tafadhalini, mpeni amwoe.

9. Mkaoane na sisi, mtupe sisi binti zenu, nanyi mkatwae binti zetu.

10. Nanyi mtakaa nasi, na nchi hii itakuwa mbele yenu; kaeni, na kufanya biashara humo, mkapate mali humo.

11. Shekemu akamwambia babaye yule msichana na nduguze, Na nikubalike machoni penu, na mtakavyoniambia nitatoa.

12. Mjapoongeza sana mahari na zawadi, nitatoa kadiri ya mtakavyoniambia, lakini mnipe huyu msichana, awe mke wangu.

13. Wana wa Yakobo wakawajibu Shekemu na Hamori babaye, kwa hila, maana amemharibu Dina, umbu lao,

14. wakawaambia, Hatuwezi kufanya neno hili, tumpe umbu letu mtu asiyetahiriwa; ingekuwa aibu kwetu.

15. Lakini kwa sharti hii tu tutapatana nanyi; mkiwa kama sisi, akitahiriwa kila mwanamume wenu,

16. ndipo tutawapa ninyi binti yetu, na sisi tutatwaa binti zenu tutakaa pamoja nanyi, nasi tutakuwa watu wamoja.

17. Lakini kama hamtusikii na kutahiriwa, basi tutamtwaa umbu letu, nasi tutakwenda zetu.

Mwa. 34