11. Uniokoe sasa na mkono wa ndugu yangu, mkono wa Esau, maana mimi namwogopa, asije akanipiga, na mama pamoja na wana.
12. Nawe ulisema, Hakika nitakutendea mema, nami nitafanya uzao wako uwe kama mchanga wa bahari, usiohesabika kwa kuwa mwingi.
13. Akakaa huko usiku ule. Kisha akatwaa baadhi ya vitu alivyokuwa navyo, kuwa zawadi kwa Esau, nduguye;
14. mbuzi wake mia mbili, na mbuzi waume ishirini, kondoo wake mia mbili, na kondoo waume ishirini;
15. ngamia wanyonyeshao thelathini pamoja na wana wao, ng’ombe wake arobaini na mafahali kumi; punda wake ishirini na wana wao kumi.
16. Akawatia mkononi mwa watumwa wake, kila kundi peke yake. Naye akawaambia watumwa wake, Vukeni mbele yangu, mkaache nafasi kati ya kundi na kundi.
17. Akamwagiza yule wa kwanza akasema, Esau, ndugu yangu, akikukuta, na kukuuliza, akisema, Wewe u wa nani? Unakwenda wapi? Tena ni wa nani hawa walio mbele yako?
18. Basi, useme, Ni wa mtumwa wako, Yakobo, ni zawadi, aliyompelekea bwana wangu, Esau. Na tazama, yeye mwenyewe yuko nyuma yetu.
19. Akamwagiza tena wa pili, na wa tatu, wote waliofuata makundi, akisema, Hivi ndivyo mtakavyomwambia Esau, akiwakuta.
20. Tena semeni, Tazama, mtumwa wako, Yakobo, yuko nyuma yetu. Maana alisema, Nitamsuluhisha kwa zawadi inayonitangulia, baadaye nitamwona uso wake; huenda atanikubali uso wangu.