Mwa. 31:15-29 Swahili Union Version (SUV)

15. Hakutufanya kama wageni, maana ametuuza, naye amekula fedha zetu kabisa?

16. Maana mali yote ambayo Mungu amemnyang’anya baba yetu, mali hiyo ndiyo yetu na ya wana wetu. Basi yo yote Mungu aliyokuambia, uyafanye.

17. Ndipo Yakobo akaondoka, akapandisha wanawe na wakeze juu ya ngamia.

18. Akachukua wanyama wake wote, na mali yake yote aliyokuwa ameyapata, na wanyama aliowapata katika Padan-aramu, ili afike kwa Isaka babaye katika nchi ya Kanaani.

19. Basi Labani alikuwa amekwenda kuwakata manyoya kondoo zake, na Raheli akaviiba vinyago vya babaye.

20. Yakobo akamhadaa Labani, Mshami, kwa kuwa hakumwambia ya kwamba anakimbia.

21. Basi akakimbia yeye na yote aliyokuwa nayo; akaondoka akauvuka mto, akaelekeza uso wake kwenda mlima wa Gileadi.

22. Hata siku ya tatu Labani akaambiwa ya kwamba Yakobo amekimbia,

23. akatwaa ndugu zake pamoja naye, akamfuata mwendo wa siku saba. Akampata katika mlima wa Gileadi.

24. Mungu akamjia Labani, Mshami, katika ndoto ya usiku, akamwambia, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari.

25. Labani akamfikia Yakobo, na Yakobo alikuwa amepiga hema zake katika mlima, na Labani na ndugu zake wakapiga hema zao katika mlima wa Gileadi.

26. Labani akamwambia Yakobo, Umefanya nini? Umenihadaa, ukawachukua binti zangu kama mateka waliotwaliwa kwa upanga.

27. Mbona umekimbia kwa siri ukanihadaa, wala hukuniambia, nipate kuagana nawe uende zako kwa furaha, na nyimbo, na ngoma, na kinubi?

28. Wala hukuniacha niwabusu wanangu, na binti zangu; basi umetenda upumbavu.

29. Ninao uwezo mkononi mwangu wa kukufanyia madhara; lakini Mungu wa baba yako usiku huu ameniambia, akisema, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari.

Mwa. 31