Mwa. 31:1-11 Swahili Union Version (SUV)

1. Basi Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu; na kwa mali ya baba yetu amepata fahari hii yote.

2. Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama jana na juzi.

3. BWANA akamwambia Yakobo, Urudi mpaka nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe.

4. Yakobo akatuma watu, akawaita Raheli na Lea waje nyikani kwenye wanyama wake. Akawaambia,

5. Naona uso wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama jana na juzi. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami.

6. Nanyi mmejua ya kwamba kwa nguvu zangu zote nimemtumikia baba yenu.

7. Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara wangu mara kumi; lakini Mungu hakumwacha kunidhuru.

8. Aliposema, Walio na madoadoa watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema, Walio na milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia.

9. Hivi Mungu akamnyang’anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi.

10. Ikawa, wakati wale wanyama walipochukua mimba, naliinua macho yangu nikaona katika ndoto, na tazama, mabeberu waliowapanda hao wanyama walikuwa na milia, na madoadoa, na marakaraka.

11. Na malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi hapa.

Mwa. 31