Mwa. 30:15-26 Swahili Union Version (SUV)

15. Naye akamwambia, Je! Ni jambo dogo kuninyang’anya mume wangu; hata wataka kuzitwaa tunguja za mwanangu pia? Raheli akamwambia, Kwa hiyo atalala kwako usiku huu kwa tunguja za mwanao.

16. Yakobo akaja kutoka kondeni jioni, Lea akatoka kumlaki, akasema, Lazima uje kwangu, kwa sababu nimekuajiri, kwa tunguja za mwanangu; akalala kwake usiku ule.

17. Mungu akamsikia Lea, naye akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana wa tano.

18. Lea akasema, Mungu amenipa ujira wangu, kwa sababu nimempa mume wangu mjakazi wangu. Akamwita jina lake Isakari.

19. Lea akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa sita.

20. Lea akasema, Mungu amenipa mahari njema, sasa mume wangu atakaa nami, kwa kuwa nimemzalia wana sita. Akamwita jina lake Zabuloni.

21. Baadaye akazaa binti, akamwita jina lake Dina.

22. Mungu akamkumbuka Raheli; Mungu akamsikia, akamfungua tumbo.

23. Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, Mungu ameondoa aibu yangu.

24. Akamwita jina lake Yusufu, akisema, Bwana aniongeze mwana mwingine.

25. Ikawa Raheli alipomzaa Yusufu, Yakobo akamwambia Labani, Nipe ruhusa niende kwetu, na kwenye nchi yangu.

26. Nipe wake zangu na watoto wangu, niliokutumikia, niende zangu, maana umejua utumishi wangu niliokutumikia.

Mwa. 30