7. Akasema, Tazama, ukali mchana bado, wala sio wakati wa kukusanya wanyama; wanywesheni kondoo, mwende kuwalisha.
8. Wakasema, Hatuwezi, hata yakusanyike makundi yote, watu wakafingirishe jiwe katika kinywa cha kisima, ndipo tunapowanywesha kondoo.
9. Hata alipokuwa akisema nao, Raheli akaja na kondoo za baba yake, maana aliwachunga.
10. Ikawa Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mamaye, na kondoo za Labani, ndugu wa mamaye, Yakobo akakaribia, na kulifingirisha lile jiwe litoke katika kinywa cha kisima, akawanywesha kondoo za Labani, ndugu wa mamaye.
11. Yakobo akambusu Raheli, akainua sauti yake akalia.
12. Yakobo akamwarifu Raheli ya kuwa yeye ni ndugu wa babaye, na ya kuwa ni mwana wa Rebeka. Basi akapiga mbio akampasha babaye habari.
13. Ikawa Labani aliposikia habari za Yakobo, mwana wa nduguye, akaenda mbio amlaki, akamkumbatia, akambusu, akamleta nyumbani kwake. Naye akamwambia Labani maneno hayo yote.