Mwa. 27:24-34 Swahili Union Version (SUV)

24. Akamwuliza, Wewe ndiwe kweli mwanangu Esau? Akasema, Ndimi.

25. Akasema, Niletee karibu nami nipate kula mawindo ya mwanangu, ili roho yangu ikubariki. Akamsogezea karibu, naye akala; kisha akamletea mvinyo, akanywa.

26. Isaka, baba yake, akamwambia, Njoo karibu sasa, ukanibusu, mwanangu.

27. Akakaribia akambusu. Naye akasikia harufu ya mavazi yake, akambariki akasema,Tazama, harufu ya mwananguNi kama harufu ya shamba alilolibariki Bwana.

28. Mungu na akupe ya umande wa mbingu,Na ya manono ya nchi,Na wingi wa nafaka na mvinyo.

29. Mataifa na wakutumikieNa makabila wakusujudie,Uwe bwana wa ndugu zako,Na wana wa mama yako na wakusujudie.Atakayekulaani alaaniwe,Na atakayekubariki abarikiwe.

30. Ikawa Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, na alipokuwa Yakobo ndiyo kwanza ametoka mbele ya Isaka, baba yake, mara Esau ndugu yake akaja kutoka katika kuwinda kwake.

31. Naye pia amefanya chakula kitamu akamletea babaye, akamwambia baba yake. Babangu na aondoke, ale mawindo ya mwanawe, ili roho yako inibariki.

32. Isaka, baba yake, akamwuliza, U nani wewe? Akasema, Mimi ni mwanao, Esau, mzaliwa wako wa kwanza.

33. Isaka akatetemeka tetemeko kuu sana, akasema, Ni nani basi yule aliyetwaa mawindo akaniletea? Nami nimekwisha kula kabla hujaja wewe, nikambariki; naam, naye atabarikiwa.

34. Esau aliposikia maneno ya babaye, akalia kilio kikubwa cha uchungu sana, akamwambia babaye, Nibariki na mimi, mimi nami, Ee babangu.

Mwa. 27