Mwa. 26:22-35 Swahili Union Version (SUV)

22. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.

23. Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba.

24. BWANA akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu.

25. Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko.

26. Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake.

27. Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu?

28. Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba BWANA alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe

29. ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa BWANA.

30. Basi akawafanyia karamu, nao wakala, wakanywa.

31. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaapiana wao kwa wao, kisha Isaka akawapa ruhusa, nao wakaenda zao kwa amani.

32. Ikawa siku ileile, watumwa wa Isaka wakaja wakampasha habari za kile kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, Tumeona maji.

33. Naye akakiita jina lake Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba, hata leo.

34. Esau alipokuwa mwenye miaka arobaini, akamwoa Yudithi, binti Beeri, Mhiti, na Basemathi, binti Eloni, Mhiti.

35. Roho zao Isaka na Rebeka zikajaa uchungu kwa ajili yao.

Mwa. 26