20. Isaka akawa mwenye miaka arobaini alipomtwaa Rebeka binti Bethueli, Mshami, wa Padan-aramu, ndugu wa Labani, Mshami, kuwa mke wake.
21. Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba.
22. Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA.
23. BWANA akamwambia,Mataifa mawili yako tumboni mwako,Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako.Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili,Na mkubwa atamtumikia mdogo.
24. Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake.
25. Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau.
26. Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake unamshika Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa.
27. Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa nyikani, na Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa hemani.
28. Basi Isaka akampenda Esau, kwa sababu alikula mawindo yake, na Rebeka akampenda Yakobo.
29. Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana.
30. Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu.