Mwa. 24:56-67 Swahili Union Version (SUV)

56. Naye akawaambia, Msinikawilishe, mradi BWANA amefanikisha njia yangu; nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu.

57. Wakasema, Na tumwite huyo msichana, tumwulize mwenyewe.

58. Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je! Utakwenda na mtu huyu? Akasema, Nitakwenda.

59. Ndipo wakampeleka Rebeka ndugu yao, na yaya wake, na mtumishi wa Ibrahimu, na watu wake.

60. Wakambarikia Rebeka, wakamwambia, Ndugu yetu, uwe wewe mama wa kumi elfu, mara elfu nyingi, na wazao wako waurithi mlango wa hao wawachukiao.

61. Rebeka akaondoka na vijakazi wake, nao wakapanda juu ya ngamia, wakamfuata yule mtu. Naye huyo mtumishi akamchukua Rebeka akaenda zake.

62. Basi Isaka alikuwa amekuja kwa njia ya Beer-lahai-roi, maana alikaa katika nchi ya kusini.

63. Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja.

64. Rebeka akainua macho, naye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia.

65. Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika.

66. Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda.

67. Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamake.

Mwa. 24