Mwa. 24:42-50 Swahili Union Version (SUV)

42. Nami nikaja leo kisimani, nikasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ukinifanikishia sasa njia yangu niendayo mimi,

43. tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji; basi na iwe hivi, msichana ajaye kuteka maji, nikamwambia, Nipe, nakuomba, maji kidogo katika mtungi wako ninywe,

44. naye akaniambia, Unywe wewe, na ngamia zako pia nitawatekea, huyo na awe ndiye mke BWANA aliyemwekea mwana wa bwana wangu.

45. Hata kabla sijaisha kusema moyoni mwangu, tazama! Rebeka akatokea, na mtungi begani mwake. Akashuka kisimani akateka. Nami nikamwambia, Tafadhali nipe maji ninywe.

46. Akafanya haraka akatua mtungi wake chini, akanena, Unywe, na ngamia zako nitawanywesha pia; basi nikanywa, akawanywesha na ngamia nao.

47. Kisha nikamwuliza nikasema, U binti wa nani wewe? Naye akasema, Mimi ni binti Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia. Nami nikamtia hazama puani mwake na vikuku mikononi mwake.

48. Nikainama, nikamsujudia BWANA, nikamtukuza BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, aliyeniongoza njiani, nimtwalie mwana wa bwana wangu binti wa ndugu yake.

49. Basi, kama mnataka kumfanyia rehema na kweli bwana wangu, niambieni kama sivyo, niambieni; ili nigeuke upande wa kuume au wa kushoto.

50. Ndipo Labani na Bethueli wakajibu wakasema, Neno hili limetoka kwa BWANA, wala sisi hatuwezi kukuambia neno jema wala baya.

Mwa. 24