Mwa. 24:35-49 Swahili Union Version (SUV)

35. na BWANA amembarikia sana bwana wangu, amekuwa mtu mkuu; amempa kondoo, na ng’ombe, na fedha, na dhahabu, na watumwa, na wajakazi, na ngamia, na punda.

36. Naye Sara, mkewe bwana wangu, akamzalia bwana wangu mwana wa kiume, katika uzee wake; naye amempa yote aliyo nayo.

37. Kisha bwana wangu akaniapisha akisema, Usimtwalie mwanangu mke wa binti za Wakanaani, ambao nakaa katika nchi yao.

38. Ila uende mpaka nyumbani kwa babangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu mke.

39. Nikamwambia bwana wangu, Labda huyo mwanamke hatafuatana nami.

40. Akaniambia, BWANA, ambaye naenenda machoni pake, atapeleka malaika wake pamoja nawe, atafanikisha njia yako; nawe umtwalie mwanangu mke katika jamaa zangu, na wa nyumba ya babangu.

41. Ndipo utafunguliwa kiapo changu hapo utakapowafikilia jamaa zangu; nao wasipokupa msichana huyo, utafunguliwa kiapo changu.

42. Nami nikaja leo kisimani, nikasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ukinifanikishia sasa njia yangu niendayo mimi,

43. tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji; basi na iwe hivi, msichana ajaye kuteka maji, nikamwambia, Nipe, nakuomba, maji kidogo katika mtungi wako ninywe,

44. naye akaniambia, Unywe wewe, na ngamia zako pia nitawatekea, huyo na awe ndiye mke BWANA aliyemwekea mwana wa bwana wangu.

45. Hata kabla sijaisha kusema moyoni mwangu, tazama! Rebeka akatokea, na mtungi begani mwake. Akashuka kisimani akateka. Nami nikamwambia, Tafadhali nipe maji ninywe.

46. Akafanya haraka akatua mtungi wake chini, akanena, Unywe, na ngamia zako nitawanywesha pia; basi nikanywa, akawanywesha na ngamia nao.

47. Kisha nikamwuliza nikasema, U binti wa nani wewe? Naye akasema, Mimi ni binti Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia. Nami nikamtia hazama puani mwake na vikuku mikononi mwake.

48. Nikainama, nikamsujudia BWANA, nikamtukuza BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, aliyeniongoza njiani, nimtwalie mwana wa bwana wangu binti wa ndugu yake.

49. Basi, kama mnataka kumfanyia rehema na kweli bwana wangu, niambieni kama sivyo, niambieni; ili nigeuke upande wa kuume au wa kushoto.

Mwa. 24