7. Akasema, N’nani angemwambia Ibrahimu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake.
8. Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya.
9. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka.
10. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka.
11. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe.
12. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.
13. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako.
14. Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba.
15. Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja.
16. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia.
17. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko.
18. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa.